NGUVU YA MUNGU KATIKA UDHAIFU WETU

SOMO: NGUVU YA KRISTO KATIKA UDHAIFU WETU

Andiko Kuu: 2 Wakorintho 12:1–10. “Neema yangu yakutosha; kwa maana nguvu yangu hukamilika katika udhaifu.” (2 Wakorintho 12:9)

UTANGULIZI

Wapendwa katika Kristo Yesu, maisha ya Mkristo siyo safari ya raha na mafanikio ya kila siku, bali ni njia yenye majaribu, udhaifu, na maumivu, ambamo Mungu anajifunua kwa namna ya ajabu.
Mtume Paulo anatufundisha kwamba udhaifu si kushindwa, bali ni mwangalizo wa nafasi ya nguvu ya Mungu kufanya kazi ndani yetu.

MAANA YA UDHAIFU KIBIBLIA.

Udhaifu ni Kukosa Uwezo wa Kujitegemea Bila Mungu

Biblia inafundisha kwamba udhaifu wa kweli ni kutambua kwamba bila Mungu hatuwezi chochote.

📖 Yohana 15:5 “Mimi ni mzabibu, ninyi matawi; akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana; kwa maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno lo lote.”

Hivyo udhaifu sio tu hali ya kushindwa, bali ni kutambua uhalisia wetu wa kibinadamu — kwamba nguvu, hekima, na uhai wote hutoka kwa Mungu. Na kutambua udhaifu huleta unyenyekevu ndani yetu kwa Mungu wetu

Kwa Kigiriki neno linalotumika katika 2 Wakorintho 12:9 ni “astheneia” likimaanisha: kutokuwa na nguvu, kutokuwa na uwezo, au hali ya udhaifu wa kimwili, kiroho, au kihisia.

1. MUNGU HUFUNUA SIRI KWA WANYENYEKEVU

📖 2 Wakorintho 12:1–4. Paulo alipata ufunuo wa mbinguni ya tatu, lakini hakujivuna — alikaa mnyenyekevu. Mungu alijua moyo wake na alihakikisha Paulo anabaki katika unyenyekevu kwa kumpa “mwiba katika mwili.”

Maandiko ya Kusaidia:

  • Yakobo 4:6: “Mungu huwapinga wenye kiburi, bali huwapa neema wanyenyekevu.”
  • Mithali 11:2: “Kujivuna huleta aibu, bali hekima iko kwa wanyenyekevu.”

Funzo:
Watu wengi wanapobarikiwa na ufunuo, au karama, huanza kujisifu kana kwamba ni kwa uwezo wao. Mungu, kwa hekima yake, huwaruhusu kupitia mambo yanayowakumbusha kuwa bado ni wanadamu. Hivyo, unyenyekevu ni kinga dhidi ya kuanguka kiroho.

2. MWIBA KATIKA MWILI NI SEHEMU YA SAFARI YA IMANI

📖 2 Wakorintho 12:7–8. Paulo alipewa “mwiba” ili asijiinuwe kupita kiasi. Haijulikani hasa ulikuwa ni ugonjwa, mateso, au mapambano ya kiroho — lakini ilikuwa ni hali iliyomtesa sana.

Maandiko ya Kusaidia:

  • Ayubu 23:10: “Lakini ajua njia nitembeayo; akishanijaribu, nitatoka kama dhahabu.”
  • Zaburi 119:71: “Imenifaa kuteseka, ili nipate kujifunza maagizo yako.”
  • Warumi 8:28: “Na tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao kwa mema.”

Funzo:
Kuna mateso ambayo Mungu huruhusu si kwa adhabu, bali kwa mafunzo ya kiroho.
Mwiba unatusaidia tusisahau tunamtegemea Mungu, si sisi wenyewe.
Kama vile dhahabu inavyosafishwa kwa moto, vivyo hivyo imani yetu inakua kupitia majaribu.

3. MAOMBI YASIYOJIBIWA KWA NJIA TUNAYOTARAJIA: Maombi yakizanayo na kusudi la Mungu

📖 2 Wakorintho 12:8. Paulo aliomba mara tatu Bwana auondoe ule mwiba, lakini Mungu hakufanya hivyo. Badala yake alimjibu: “Neema yangu yakutosha.”

Maandiko ya Kusaidia:

  • Yesu mwenyewe aliomba: “Baba, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” (Mathayo 26:39)
  • Isaya 55:8–9: “Mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu.”

Funzo:
Kuna wakati Mungu hatusikilizi kwa namna tunavyotaka, kwa sababu anajua kilicho bora zaidi kwa roho zetu.
Mungu hutupa kile tunachohitaji, si kila tunachotaka.
Hivyo, maombi kutojibiwa si dalili ya Mungu kutusahau — ni dalili kwamba mpango wake ni mkuu kuliko wetu.

4. NGUVU YA KRISTO HUKAMILIKA KATIKA UDAHAIFU

📖 2 Wakorintho 12:9–10 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu”

Paulo anasema: “Ndio maana napendezwa na udhaifu… kwa maana nikiwa dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”  Hapa tunajifunza kanuni kuu ya kiroho:  Wakati tunapokuwa hatuna uwezo wetu, ndipo nguvu ya Mungu inapata nafasi ya kufanya kazi kikamilifu.

Maandiko ya Kusaidia:

  • Filipi 4:13: “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”
  • Isaya 40:29–31: “Huwapa nguvu wazimiao, humwogezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo… watapanda kwa mbawa kama tai.”
  • Habakuki 3:17–19: Hata kama miti haitoi matunda, bado nitamshangilia Bwana — kwa maana “Bwana MUNGU ndiye nguvu yangu.”
  • Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu; kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo…” Udhaifu wa kiroho unamhitaji Roho Mtakatifu atupe nguvu ya kusimama na kuomba, maana bila Yeye tunashindwa.

Funzo:
Nguvu ya Mungu haionekani katika wakati wa amani tu, bali hasa katika nyakati za udhaifu, magumu, na majaribu.
Kama mafuta yanavyotoa mwanga yanapochomwa, vivyo hivyo nuru ya Kristo inang’aa zaidi ndani yetu tunapokuwa dhaifu.

5. MFANO WA WATU WA MUNGU WALIOONA NGUVU KATIKA UDAHAIFU

  • Musa: Alijiona si msemaji mzuri (Kutoka 4:10), lakini Mungu alimtumia kuwakomboa Israeli.
  • Gideoni: Alijiona duni (Waamuzi 6:15), lakini Mungu alimfanya shujaa.
  • Daudi: Alikuwa mchungaji mdogo, lakini Mungu alimfanya mfalme.
  • Petro: Alimkana Yesu mara tatu, lakini baadaye akawa mhubiri mwenye nguvu Mathayo 26:33-35, 69-75, Mdo 2:1-40

Funzo:
Mungu hapendi watu “wenye nguvu zao,” bali wale wanaotambua udhaifu wao na kumruhusu Kristo na Roho Mtakatifu kuwa nguvu yao.

HITIMISHO:- Udhaifu ni Wito wa Kutegemea Neema ya Mungu

📖 2 Wakorintho 12:9-10 “Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu; Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”

Kwa hiyo, udhaifu ni nafasi ya Mungu kujionyesha mwenyewe kuwa Yeye ni Nguvu yetu.
Kadiri tunavyokuwa wanyonge, ndivyo Kristo anavyotukamilisha. Tunapokubali kwamba hatuwezi bila Mungu, ndipo anapoweza kufanya kazi kwa ukamilifu ndani yetu.

Imeandaliwa na : –

Mwl: Anselemi Mashimba Alloyce

Mwalimu wa Neno la Mungu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *