SOMO: UTUMISHI KATIKA UFALME WA MUNGU

lengo:

1: kuelewa Msingi wa wito wa utumishi wa Kiroho

2: kuelewa sifa na tabia zinazopaswa kuonekana kwa mtumishi wa kiroho Kristo akiwa kielelezo na kigezo.

3: kuelewa changamoto, thawabu na hatima ya utumishi wa kiroho


🔹MADA: MSINGI NA WITO WA UTUMISHI

Lengo la Siku ya Kwanza

  • Kuelewa maana halisi ya utumishi wa Kikristo
  • Kutambua kuwa kila Mkristo ameokoka ili atumike
  • Kuweka msingi wa kibiblia wa utumishi

1. Maana ya Utumishi wa Kikristo

Utumishi wa Kikristo ni:

  • Kujitoa kwa Mungu kwa moyo wote. Warumi 12:1
  • Kutimiza mapenzi ya Mungu kwa kuwahudumia watu. Zaburi 40:8; Yohana 4:34, 5:30, 6:38
  • Kuishi kwa ajili ya Kristo, si kwa ajili ya nafsi. 2 Wakorintho 5:15; Wagalatia 2:20

Fundisho kuu: Utumishi ni mwitikio wa wokovu, si njia ya kuupata wokovu.

2. Chanzo cha Utumishi: Wito wa Mungu

Hakuna mtu anayetumika bila kuitwa.

Waebrania 5:4 – Hakuna mtu ajitwaliaye heshima hii
Yeremia 1:5 – Kabla hujazaliwa nalikujua
Yohana 15:16 – Sinyi mlionichagua, bali mimi niliwachagua

Yapo Mambo ya msingi katika Utumishi

👉 Utumishi:

  • Una wito (calling)
  • Una kusudi (purpose)
  • Una mpango (assignment)

1. WITO (CALLING)

Maana ya Wito

Wito ni mwito wa Mungu kwa mtu kuingia katika maisha ya kumtumikia Yeye.
Ni uamuzi wa Mungu, si wa mwanadamu. Wito hutangulia huduma, vipawa, au ofisi.

“Si ninyi mlionichagua, bali mimi niliwachagua ninyi…” (Yohana 15:16)

Asili ya Wito

  • Wito unatoka kwa Mungu (Waebrania 5:4)
  • Ni wa neema, si matendo (Warumi 11:29)
  • Huambatana na uwajibikaji mkubwa (Yakobo 3:1)

Aina za Wito

  1. Wito wa wokovu – kila mtu (2 Petro 3:9)
  2. Wito wa jumla wa utumishi – waamini wote (1 Petro 2:9)
  3. Wito maalum – huduma fulani (Yeremia 1:5; Wagalatia 1:15)

Sifa za Wito

  • Hauondolewi kirahisi. Angalia kwa Yona anajaribu kukimbia lakini BWANA anamfuatilia. Soma Yona yote
  • Huleta mzigo wa rohoni. “Utawezaje kutulia, ikiwa BWANA amekupa agizo?” (Yeremia 47:7)
  • Huonekana hata kabla ya mtu kujitambua (Paulo – Matendo 9)

📌 Bila wito → huduma huwa kazi ya kibinadamu, si ya kiroho.

2. KUSUDI (PURPOSE)

Maana ya Kusudi

Kusudi ni sababu kuu kwa nini Mungu anakuita. Ni “kwa ajili ya nini?” ya utumishi wako.

“Kwa maana sisi tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu tupate kutenda matendo mema…” (Waefeso 2:10)

Kusudi Hutofautiana na Wito

  • Wito ni mwito wa kuwa mtumishi
  • Kusudi ni sababu ya utumishi huo

Mifano ya Kusudi

  • Musa – kuwaokoa Israeli (Kutoka 3:10)
  • Yeremia – kuwa nabii wa mataifa (Yeremia 1:5)
  • Paulo – kupeleka Injili kwa Mataifa (Matendo 9:15)

Kusudi Huleta:

  1. Mwelekeo – kutambua cha kufanya
  2. Motisha – nguvu ya kuendelea
  3. Mipaka – hukusaidia kusema hapana kwa mambo yasiyo yako

“Nitakimbia kuelekea shabaha…” (Wafilipi 3:14)

📌 Bila kusudi → utumishi huwa wa kuhangaika bila matokeo ya kudumu.

3. MPANGO (ASSIGNMENT)

Maana ya Mpango

Mpango ni kazi au jukumu maalum Mungu analokupa kwa wakati, mahali, na watu fulani.
Mpango unaweza kubadilika, lakini wito hubaki.

“Kuna wakati wa kila jambo…” (Mhubiri 3:1)

Mpango Hutegemea:

  • Mahali (location)
  • Wakati (season)
  • Kiwango cha ukuaji wa mtumishi

Mifano ya Mpango

  • Daudi:
    • Kwanza mchungaji wa kondoo
    • Baadaye shujaa
    • Hatimaye mfalme
  • Paulo:
    • Antiokia
    • Safari za kimisionari
    • Hatimaye gerezani akiandika nyaraka

Sifa za Mpango

  • Hubadilika kulingana na msimu.
  • Huhitaji utiifu wa sasa. “Nalifanya haraka wala sikukawia, kuyatii maagizo yako” (Zaburi 119:60)
  • Huthibitishwa na matunda (Matendo 13:2–3)

📌 Tatizo kubwa: watu wengi wanapenda mpango bila kuelewa wito na kusudi.

MUHTASARI WA TOFAUTI

KipengeleMaelezoHubadilika?
WitoMwito wa Mungu kuwa mtumishi❌ Hapana
KusudiSababu ya kuitwa❌ Mara chache
MpangoKazi/eneo maalum kwa wakati✅ Ndiyo

HITIMISHO

✔ Wito → NANI umeitwa kuwa
✔ Kusudi → KWA NINI umeitwa
✔ Mpango → NINI unafanya sasa

“Mtu aitwaye na Bwana, na aendelee katika wito wake.” (1 Wakorintho 7:20)

3. Kila Muumini Ameitwa Kutumika

Hakuna Mkristo “mtazamaji” katika ufalme wa Mungu.

1 Petro 2:9 – Ukuhani wa kifalme
1 Petro 4:10 – Kila mmoja na karama yake
Waefeso 4:7 – Neema imepewa kila mmoja

Hitimisho la siku ya kwanza:
👉 Kama umeokoka, umeitwa kutumika.


🔹 SIKU YA PILI: Ijumaa 16/01/2026

MADA: MFANO WA YESU NA TABIA ZA MTUMISHI WA KWELI

Lengo la Siku ya Pili

  • Kumtazama Yesu kama kigezo cha utumishi
  • Kujifunza tabia za lazima za mtumishi
  • Kufahamu gharama ya utumishi

1. Yesu Kristo – Mtumishi Mkamilifu

Yesu ni Bwana, lakini alichagua kuwa mtumishi.

Marko 10:45 – Hakuja kuhudumiwa bali kuhudumia
Wafilipi 2:5–8 – Alitwaa mfano wa mtumwa
Isaya 53:11 – Mtumishi wangu mwenye haki

Ebrania 12:1-3  Tumtazame Yesu aliyestahimili mapingamizi

Mfano wa vitendo: Yohana 13:3–15 – Yesu ananawisha miguu ya wanafunzi

👉 Hakuna kazi ndogo katika utumishi wa kweli.

2. Tabia za Mtumishi wa Kweli

(a) Unyenyekevu. Mathayo 23:11–12; Yakobo 4:10

(b) Uaminifu. 1 Wakorintho 4:1- 2; Mathayo 25:21

(c) Utii. 1 Samweli 15:22; Yohana 14:15

(d) Upendo.  1 Wakorintho 13:1–3; Yohana 13:34–35

3. Gharama ya Utumishi

Utumishi wa kweli una gharama. Hivyo ni muhimu kujua ili tusijeshindwa Luka 14:25-33

  1. Kujikana nafsi: Luka 9:23. Hapa ni kule kukubali kufa yaani kuufisha utu wa kale Kol 2:20, 3:1-5
  2. Kupata mateso kwa ajili ya Kristo: 2 Timotheo 3:12, Mdo 16:23, 2 Kor 11:23, kol 1:24-25; 2 Wakorintho 6:4–10 – Paulo aeleza mateso ya utumishi

👉 Usipotaka gharama, hujawa tayari kwa utumishi.


🔹 SIKU YA TATU: Shule ya Jumapili 19/01/2026

MADA: CHANGAMOTO, TUZO NA HATIMA YA UTUMISHI

Lengo la Siku ya Tatu

  • Kuelewa changamoto za utumishi
  • Kujua jinsi ya kudumu katika utumishi
  • Kutambua thawabu za milele za utumishi

1. Changamoto Katika Utumishi

Kama mtumishi wa Mungu utakutana na changamoto zenye lengo la kuyateteresha maadili yako na Imani yako. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto hizo

  1. Upinzani na Chuki: – Hata unapofanya mema, unaweza kukutana na watu wasiokuelewa na wakakupinga. “Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mathayo 10:22)
  2. Kishawishi cha kiburi: Unapofanikiwa kuna hatari ya kujitwalia utukufu badala ya kumrudishia Mungu. “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu” (Mithali 11:2),
  3. Uchovu wa mwili na roho (Burnout): – Kuna hali ya kuchoka kimwili kutokana na mambo mengi ambayo yanaweza kukukabili katika utumishi.Marko 6:31, Isaya 40:29 – 31
  4. Kukata tamaa: – Mtumishi anweza kuchoka na kukata tamaa anapoona matunda hayaji upesi. “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho” (Gal 6:9), Luka 18:1
  5. Mashambulizi ya adui: – Mtumishi daima yupo katika vita na shetani katika ulimwengu wa roho hivyo anawindwa daima na shetani akimzungukia daima hivyo kuwa makini sana mtengemee Mungu daima. 1 Petro 5:8-9

Namna ya Kudumu Katika Utumishi

  1. Kaa ndani ya Yesu Kristo:- Yohana 15:4–5
  2. Mtegemee Kristo daima: Waebrania 12:1–3
  3. Tumia kwa halali neno la Kweli (Kristo): – 2 Timotheo 2:15

Msingi wa kudumu:

  • Maombi
  • Neno
  • Ushirika
  • Unyenyekevu

2. Tuzo/thawabu za Utumishi

 (Biblia inafundisha kuwa utumishi haupotei bure) Kol 3:24-25, Marko 10:29 – 30  

“Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake…” – Waebrania 6:10

MISINGI YA KIBIBLIA YA TUZO

(a) Mungu ni Mlipaji wa Huduma: Utumishi wote wa kweli una malipo kutoka kwa Mungu, si lazima kwa wanadamu.

“Basi thawabu yako itakuwa kubwa.” (Luka 6:35)

“Baba yako aonae sirini atakulipa.” (Mathayo 6:4)

📌 Utumishi usiotambuliwa na watu bado unatambuliwa na Mungu.

(b) Tuzo si wokovu: Ni muhimu kufahamu:

  • Wokovu ni kwa neema (Waefeso 2:8–9)
  • Tuzo ni kwa uaminifu katika utumishi (1 Wakorintho 3:8) “Kila mtu atapokea thawabu yake mwenyewe, kwa kadiri ya kazi yake.”

AINA ZA TUZO ZA UTUMISHI

Tuzo/thawabu za kiroho zinaanza hapa duniani kupitia baraka, lakini kilele chake  ni mbinguni.

A. TUZO ZA SASA (DUNIANI)

Hizi hutolewa na Mungu wakati mtu bado yuko duniani.

1. Furaha na Amani ya Ndani: Mtumishi wa kweli hupokea furaha isiyohusiana na mazingira.

“Furaha ya Bwana ndiyo nguvu yenu.” (Nehemia 8:10)

“Amani ya Mungu ipitayo akili zote…” (Wafilipi 4:7)

📌 Utumishi huleta mateso, lakini pia huleta furaha ya kipekee.

2. Uthibitisho wa Mungu (Divine Approval): Mungu humshuhudia mtumishi wake kwa:

  • matunda
  • ushuhuda wa Roho
  • kuthibitisha kazi yake

“Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye.” (Mathayo 3:17)

3. Ukuaji wa Kiroho na Mamlaka: Kadiri mtu anavyotumikia kwa uaminifu:

  • hukua kiroho
  • hupewa mamlaka zaidi: utumishi wa unyenyekevu huleta kibali na kuinuliwa (Mathayo 23:11)

“Aliye mwaminifu katika yaliyo madogo…” (Luka 16:10)

4. Baraka za Mahitaji (sio anasa): Mungu hutunza watumishi wake. Mungu anaahidi kuwabariki wale wanaotumika kwa uaminifu (Kutoka 23:25)“Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu… na hayo yote mtazidishiwa.” (Mathayo 6:33).

B. TUZO ZA MBINGUNI (ZA MILELE) – Taji

Hizi ndizo tuzo kuu za utumishi. “Jiwekeni hazina mbinguni…” (Mathayo 6:20).

Tutapokea taji katika Kiti Cha Hukumu cha Kristo (Bema Seat).  Hapa si hukumu ya wokovu, bali ya tuzo za kazi.

“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” — 2 Wakorintho 5:10

“…Moto utaijaribu Kazi ya kila mtu, kazi yako ikikaa utapata thawabu, ikiteketea unapata hasara( utakosa tuzo), bali utaokolewa kama kwa moto (Yaani huna kitu).” (1 Wakorintho 3:13 – 15)

📌 Kazi:

  • ya dhahabu → italipwa
  • ya majani → itateketea

 AINA YA TAJI (CROWNS) ZA KIBIBLIA

Biblia inataja aina tano ya taji kama tuzo za uaminifu.

1. Taji Isiyoharibika. Kwa wale walio na nidhamu na kujikana 1 Wakorintho 9:25

Hutolewa kwa watumishi wanaodhibiti miili yao na tamaa za dunia kwa ajili ya huduma.

2. Taji ya Furaha (Soul Winner’s Crown). Kwa wale wanaoleta watu kwa Kristo

“Maana tumaini letu, au furaha yetu, au taji ya kujionea fahari, ni nini? Je! Si ninyi, mbele za Bwana wetu Yesu, wakati wa kuja kwake?” (1 Wathesalonike 2:19).  Ni tuzo ya wahubiri, wamisionari, na mashahidi wa Injili.”Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele” (Dan 12:3)

3. Taji ya Haki. Kwa wale wanaopenda kurudi kwa Kristo 2 Timotheo 4:8

Hutolewa kwa wanaoishi maisha ya utakatifu wakingojea Bwana.

4. Taji ya Uzima. Kwa kuvumilia majaribu na mateso Yakobo 1:12; Ufunuo 2:10

Hasa kwa walioteswa kwa sababu ya imani. Kumbuka “Mateso ya mwenye haki ni mengi, lakini BWANA humponya nayo yote” (Zaburi 34:21)

5. Taji ya Utukufu isiyokauka. Kwa wachungaji, viongozi na watumishi waaminifu. 1 Petro 5:2–4

Kwa wanaochunga kondoo si kwa faida bali kwa moyo wa kuitwa.

 VIGEZO VYA KUPEWA TUZO

Mungu hatoi tuzo kwa:
❌ umaarufu
❌ ukubwa wa huduma
❌ sifa za watu

Bali kwa:
✔ uaminifu (Mathayo 25:21)
✔ nia ya moyo (1 Wakorintho 4:5, Wakolosai 3:23-24)
✔ utiifu (1 Samweli 15:22)

 HATARI YA KUPOTEZA TUZO

Mtu anaweza: kuokoka, lakini akakosa tuzo

“Akiokolewa, lakini kama kwa moto.” (1 Wakorintho 3:15)

“Shikeni sana msije mkapoteza thawabu yenu.” (2 Yohana 1:8)

NOTE:-

✔ Utumishi una gharama
✔ Lakini una tuzo ya sasa na ya milele
✔ Hakuna kazi ya Bwana isiyolipwa

“Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana siku zote kwa maana mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.” — 1 Wakorintho 15:58

  • Hatima ya Utumishi wa Kiroho

Hatima ya mtumishi wa koroho ni hesabu atakayotoa mbele ya Muumba wake kuhusu karama na nafasi alizopewa.

  1. Kuhukumiwa kwa uaminifu:- Hatima haitegemei ukubwa wa cheo, bali uaminifu katika kile kidogo ulichopewa. “Bwana akamwammbia, vema, mtumishi mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako”(Mathayo 25:21, 2 Wakorintho 5:10)
  2. Kurithishwa Ufalme:- Hatima ya mwisho ya Mtumishi wa Kweli ni kupumzika baada ya kazi ngumu ya duniani. 2 Timotheo 4:7 – 8

Hitimisho la jumla

Utumishi:

  • Ni safari, si tukio
  • Ni utiifu, si umaarufu, kwa sasa wako watu wengi wanatafuta umaarufu na Viewers kwenye mitandao
  • Ni kwa ajili ya Kristo, si wanadamu

Wakolosai 3:23–24; Yoshua 24:15. Ili mtumishi ashinde changamoto na afikie hatima njema, maandiko yanatupa siri moja kubwa: Nia ya Moyo. “Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Yesu Kristo”(Wakolosai 3: 23 – 24)

🔔 WITO WA MWISHO

👉 Mungu anatafuta watumishi waaminifu, si watu mashuhuri.